Mafunzo yetu, Ajira na Kujiajiri

By mtangoo on Jun 4, 2019 Training Views(4706)


Tangu mwaka 2014, ni miaka mitano sasa tumekuwa tukifanya mafunzo ya kitaalam na tumeona na kujifunza mengi, juu ya ajira na umuhimu wa mafunzo. Kwa Watanzania wengi wakisikia mafunzo, jambo la kwanza kufikiri ni kukaa darasani miaka kadhaa na kisha kupata cheti, iwe cha shahada ama astashahada. Sisi kama kampuni tunaikubali elimu ya darasani na tunawatia moyo wanaoweza kuipata waipate. Lakini pia tunataka Watanzania wajue ya kuwa kuna elimu nyingine, ya muhimu sana wanahitaji kuwa nayo, ili kukabiliana na dunia hii yenye changamoto ya ajira. Eneo hili ni pana, kwa hiyo nitaongelea upande wa TEHAMA na kipengele maalum cha usanifu na utengenzaji wa programu za kompyuta (Software Design and Development).

Tatizo tulilonalo kama Nchi

Tumefundisha wanafunzi wengi, baadahi wakiwa ni wanafunzi binafsi na wengine ni wafanyakazi wa taasisi na makampuni mbalimbali. Lakini pia miaka ya nyuma tulikuwa na programu maalum ya kufundisha mashuleni. Katika yote haya, katika uwepo wetu kama kampuni tumeshuhudia tatizo kubwa la ukosefu wa watenda kazi weledi katika eneo la usanifu na utengenezaji wa programu. Elimu yetu haijaweza bado kuwaandaa wanafunzi kuwa wataalamu wa eneo hili. Kuna mambo mengi wanatumia muda mwingi kuyasoma na huku hayahitajiki ama yanahitajika kwa kiwango kidogo. Lakini pia kuna mengi hawafundishwi na ni ya msingi sana huku. Kwa sababu hiyo bila juhudi binafsi, ni vigumu kwa mtu aliyemaliza shule kupata ajira au kujiajiri katika eneo hili. Anahitaji ujuzi wa ziada ili kuweza kuendana na kasi ya dunia ya ajira: iwe kwa kuajiriwa au kujiajiri

Lakini pia kuna watu ambao wako katika fani nyingine na wanaona fursa zilizo katika TEHAMA na maalum kabisa katika uandishi na usanifu wa programu, na hivyo wanataka kuongeza fani. Hawa wanapata shida ya mahali pa kujifunza, ambapo watafundishwa stadi na weledi badala ya nadharia.

Mafunzo yetu

Kwa sababu ya tatizo hili na mengine Hosanna Higher Technologies iliundwa. Tupo kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kujifunza na kujiandaa kuingia mtaani wakiwa na utaalamu, na stadi za eneo hili la fani. Lakini pia tupo kuwawezesha wamiliki wa makampuni na viongozi wa taasisi kuwa na kitengo bora cha TEHAMA kwa kuwafundisha watumishi na wafanyakazi wao, ili waweze kuendana na kasi ya teknolojia. Kwa wale wanaotaka kubadili au kuongeza fani, tupo kuwasaidia kufikia lengo hilo.

Namna ya Uendeshaji

Tunafundisha kozi mbalimbali na baadhi yake zimewekwa kwenye tovuti yetu hii. Tafadhali bonyeza hapa kuona kozi tulizo nazo kwa sasa. Katika kila kozi tuna ngazi tatu tunazofundisha. Ngazi ya kwanzani ni ya kozi ya Msingi (foundational course). Ngazi hii humsaidia yule ambaye hana ufahamu kabisa juu ya uandishi na usanifu wa programu, ama ana ufahamu wa juu juu au usio wa kiweledi juu ya kozi husika. Kozi hii inawafaa pia wale wote waliotoka shuleni na kupitiliza kazini na hawakupata nafasi ya kuijua misingi hasa ya lugha au kifaa husika.

Ngazi ya pili ni ya Kozi ya Kati (intermediate course), ambayo inalenga kumfundisha mwanafunzi juu ya kona zote anazohitaji kujua na vifaa anavyohitaji na namna ya kuvitumia ili awe mwandishi mweledi katika usanifu na uandishi wa programu. Ngazi hii ni ya juu kabisa katika mafunzo yetu na inawalenga wale ambao wana ufahamu wa msingi lakini wanatamani kufikia weledi wa juu, au taasisi na makampuni ambayo yana wasimba (programmers) ambao wangependa wawe ni wabunifu na wanaoendana na kasi ya teknolojia.

Na mwisho ni Kozi ya Wataalam (Advanced course). Kozi za ngazi hii hazikufundishi mambo mengi kama zilivyo mbili za kwanza, bali zinakufundisha eneo dogo kwa undani zaidi. Mfano unaweza kujifunza katika Kozi ya msingi namna ya kutumia mathalani Kotlin na ikakupa ufahamu wa msingi wa namna ya kuitumia kuandika programu za Android. Kisha katika ngazi ya pili ukajifunza namna ya kuandika programu bora za Android ambazo zitakutangaza na kukuletea wateja, au ambazo zitasaidia taasisi yako kuwafikia wateja kirahisi kwa teknolojia. Kwa ngazi hii ya tatu utajifunza eneo dogo sana lakini utaenda kwa undani sana. Mathalani inaweza kuwa kozi juu ya namna ya kutumia maktaba ya Jetpack inayokuja kama sehemu ya vifaa vya kutengenezea programu za Android.

Kujiunga na Kozi zetu

Kozi zetu huendeswa kwa muda maalum, na hutangazwa katika mitandao yetu ya kijamii: Facebook, Instagram, na Twitter. Pia katika kalenda yetu ya mfunzo, utakutana na ratiba ya muda mrefu. Tafadhali bonyeza hapa kuona kozi zilizopo n zijazo. Kozi ikiisha kutangazwa, inakuwa wazi kwa ajili ya kujiunga. Hatua za kujiunga ni rahisi sana. Unalipia kozi katika akaunti zetu, na kisha unatuma namba ya risiti au picha yake. Baada ya hapo utapokea ujumbe wa kujiunga kwa namba utakayokuwa umewasiliana nasi, ukiwa na maelekezo mbalimbali kuhusu kozi husika. Pia utaunganishwa katika Jukwaa maalum ambapo utaweza kupata msaada hata baada ya mafunzo, na mambo mengine. Kupata taarifa zaidi tumia kiunganishi cha "Contact" hapo juu.

Baada ya kujifunza nini kinafuata?

Ukimaliza kozi ya msingi, unaweza kuanza kufanya kazi ambazo sio kubwa. Na itakufaa kama utajiunga na kozi ngazi ya kati itakapotangazwa. Hii itakupa uwezo wa kufanya miradi mikubwa. Ukimaliza ngazi ya kati, na kufanya mazoezi sawa sawa na maelekezo ya mkufunzi wako, tunatarajia uweze kufanya miradi ya aina yote ambayo inahitaji mtu mmoja mmoja. Ukiwa na mradi unaohusisha watu wengi ni vyema timu nzima ikaangalia namna ya kupata mafunzo ya kuafanya miradi kama timu. Tuna kozi hiyo kwenye kalenda, lakini pia mnaweza kuomba kufanya kozi hiyo kwa muda na mazingira tofauti.

Kiufupi ukimaliza kozi zetu na kufuata maelekezo yote ya mkufunzi wako, tunatarajia kusikia kitu kikubwa toka kwao. Bado nchi hii ina matatizo mengi ambayo TEHAMA na kwa umaalum kabisa wasimba, tunatarajiwa kuyatatua. Kwa kuwa utatuzi wa changamoto ni fursa ya kutengeneza ajira, tunatarajia utengeneze ajira, ya kwako kwanza na kisha uwaajiri wengine. Kuna mengine unayahitaji kuwa mjasiliamali mwenye kufanikiwa katika eneo hili, lakini kwa eneo la ufundi utakuwa umepata kitu!

Mpaka wakati mwingine, nakutakia kila la kheri!

Thanks for visiting. We would like to hear your comments. If you are new here cosider to Register. If you already have an account, Please Sign in

Comments (0)